LEO kwa namna ya ajabu kabisa Bunge Maalumu la Katiba limeamua kuwanyima wananchi haki ya kujua kinaendelea nini kwa kuwazuia waandishi kushiriki katika majadiliano ya kamati.
Pamoja na kutoa sababu zao ambazo sisi tunaziona hazina mashiko, kitendo cha kuzuia mhimili wa 4 katika maisha ya kijamii ni fadhaa kwa wale wanaojua maana na umuhimu wa wapasha habari.
Pamoja na kupunguza nguvu za usahihi na ukweli, kitendo hicho kitachangia kuandika habari ambazo zinafurahisha masikio lakini hazina uhakika hasa magazeti pendwa.
Kwa upande wetu tunaona si sahihi kwa Bunge hilo kuzuiwa waandishi wa habari kwa madai kuwa watakosea na kuwapotosha wananchi. Kiukweli kwa kuwazuia hivi ndio wanakuwa na nafasi ya kutafuta ‘umbea’ na kupotosha.
Taarifa watakazopewa waandishi ni taarifa ambazo zitakuwa zimechujwa na kutooneshwa hali halisi ilivyokuwa katika kufikia hitimisho.
Hali ya kunyima haki ya kuandika na kusubiri kukariri taarifa kunaendeleza hali ile ile ya ukimya kwenye haki ya kukusanya na kupasha habari hasa katika matukio muhimu ya kitaifa kama hili la utungwaji wa Katiba mpya.
Mtu yeyote anayejua umuhimu wa wapasha habari kuwepo eneo la tukio kusaidia wananchi kuelewa mwenendo wa shughuli iliyopo mbele yao anapoona anazuiwa atajiuliza swali waheshimiwa hawa wanaogopa nini au wanataka kuficha nini kwani wananchi wana haki ya kujua kinachoendelea.
Tunapaswa tuelewe kuwa zipo sheria na kanuni za ubora wa kazi ya uandishi na waandishi wanaelewa hilo kama wanataaluma ndio maana kama wakiteleza huomba radhi na kama kukiwa na matatizo lipo Baraza lao linasaidia kutatua matatizo yaliyoonekana.
Katika mazingira ya kila mtu anataka kuwapo na uwazi na misimamo kujulikana, kitendo cha kuzuia waandishi kuingia katika kamati hizi muhimu zinazojenga msingi wa majadiliano kwenye Bunge ni dalili ya woga usiokuwa wa lazima.
Ni dhahiri hii Katiba ni ya umma na haihusiani na watawala au wanaotaka kutawala kwa namna yoyote ile, hivyo kitendo hicho cha kunyima fursa hatukishabikii kwa kuwa kinajenga hisia mbaya na msingi mbovu wa kukabiliana na masuala makubwa ya kitaifa kwa uwazi na bila jazba.
Hoja kwamba bila kamera kuna uhuru wa kuzungumza kunajenga taifa lisilojua linasimamia nini na kujaa uoga usiokuwa na mantiki.
Aidha hoja ya Mjumbe wa Kamati ya Kanuni George Simbachawene kwamba kama waandishi wa habari kwenye vikao hivyo wakiruhusiwa habari
zitatofautiana kwa kila mzungumzaji hiyo ndiyo maana halisi ya kuandika hoja ili kila mwananchi aweze kupima hoja inajengwa namna gani kwanini aje kupiga kura baadaye.
Aidha madai kuwa waandishi ni wengi kwa hiyo hawatatosha si msingi kabisa wa kuzungumza kwa tukio kubwa la kitaifa kama hili, kuwepo kwa waandishi wengi ndio kuchanua kwa demokrasia kwani kila mtu atapata haki ya kusoma kwa namna ambavyo waandishi wanachambua kinachoendelea.
Hata injili katika Biblia iliandikwa na watu wanne tofauti lakini wakibeba maudhui yale yale na hata Mungu alibariki.
Wanachotaka watu ni muafaka umefikiwaje na si taarifa ya mwisho, kwani wale ambao wataonekana kutosikilizwa ndio hao watakaotibua kabisa kwani watafikisha yaliyojiri kwa namna yao na waandishi watayaandika.
Kwetu sisi ambao kazi yetu ni daraja kati ya wananchi na watengeneza mustakabali wao sababu zilizotolewa za kuwakataa waandishi katika mikutano ya kamati ni dhaifu.
Tunaamini mchakato wa Katiba haupaswi kuwa
siri , waandishi wanapoaswa kuwa huru katika kuhabarisha umma kwani umma ndio utakaokuja kufanya maamuzi ya Katiba hii.
Ukiangalia kwa makini sababu zilizotolewa utaona kwamba wajumbe wamejazwa na hofu ambayo haina mantiki.
Tuwaangalie na wenzetu ambao hawakuwa na mpango wa kuchuja habari kwa kuzuia vyombo vya habari wakati waliporekebisha katiba zao, tuwaone Kenya na Afrika Kusini kwani wao waliruhusu waandishi.
Tunaamini hatupo vitani na hatuna sababu za kubadili uhuru wa vyombo vya habari kwani vipo kwa faida ya umma na kuwajengea maarifa ya uamuzi.