Basi la Abiria la AIR BUS lenye namba za usajili T 106 AGB, likiwa limepinduka na kutumbukia korongoni kwenye daraja la Mkange , kati ya Kijiji cha Berega na Kiegeya, wilaya ya Kilosa katika barabara kuu ya Morogoro- Dodoma , jana asubuhi, kama linavyoonakana.Katika ajali hiyo watu wanne
( Picha kwa hisani ya Mtandao wa Michuzi). WAKATI Rais Jakaya Kikwete licha ya kuelezea huzuni na masikitiko yake kufuatia vifo vya watu 39, vilivyotokea katika ajali ya barabarani wilayani Butiama , Mkoa wa Mara , ajali nyingine mbaya ya AIR Bus imetokea mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi wapatao 35.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul , alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana ( Sept 8) majira ya saa 5: 45 asubuhi katika eneo la Daraja la Mkange kati ya Kijiji cha Berega na Kiegeya , wilayani Kilosa .
Alisema ajali hiyo imepoteza maisha ya watu wanne , wanawake watatu na mwanaume mmoja ambao walifariki dunia papo hapo , ambao majina hayo hayaweza kufahamika mara moja , huku wengine 35 kujeruhiwa na walikimbizwa kwenda kupatiwa matibabu Hospitali ya Misheni ya Berega.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, kuwa basi hilo yenye namba za ujasili T 106 AGB lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Tabora na kutokana na mwendo kasi liliacha njia na kwenda kutumbukia korongoni kwenye daraja la Mkange , lililipo kati ya Kijiji cha Berega na Kiegeya, wilayani Kilosa kwenye barabara kuu ya Morogoro- Dodoma.
Hata hivyo alisema , baada ya kutokea kwa ajali hiyo dereva wa basi hilo aliyetambuliwa kwa jina la Bilal Seif alitoweka eneo hilo na Polisi ilianza msaka ili atiwe nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Mganga wa zamu wa Hospitali ya Micheni ya Berega , iliyopo kilometa kadhaa kutoka barabara kuu ya Morogoro- Dodoma katika wilaya ya Kilosa, Alfred Chiponda , alithitisha kupokea majeruhi hao 35 waliopata ajali ya basi.
Hata hivyo alisema kati ya majeruhi hao 10 ni wanawake , sita ni watoto na 19 ni wanaumme na baadhi yao wameumia vibaya kwa kuvunjika sehemu mbalimbali za mwili , wengine kichwani, kuvujika miguu ama mikono.
Kwa mujibu wa Mganga wa Hospitali hiyo , baadhi ya majeruhi walioumia vibaya wamehamishiwa kwa kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi.
Nao baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo , wakizungumza kwa nyakati tofauti walidai , dereva wa basi hilo licha ya kuwa katika mwendo kasi , pia alikuwa akitaka kulipita gari jingine lililokuwa mbele yake na kupoteza mwelekeo uliosababisha gari hilo kuacha njia na kupinduka eneo la darajani. Source:John Nditi Habarileo Morogoro |