BAADA ya kutumikia timu ya Ferrari kwa miaka 23 na kuiletea mafanikio makubwa mwenyekiti wa timu hiyo Luca Di Montezemolo anaachia ngazi katika uongozi wa timu hiyo inayoshiriki mbio za magari kasi za Formula 1 .
Kuondokana kwake kunatokana na timu hiyo kutofanya vyema katika msimu huu na pia kutokuelewana kwake na Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni mama ya Fiat Sergio Marchionne.
Mwenyekiti huyo mwenye umri wa miaka 67 amesema kwamba anafurahi kuhitimisha kazi ambayo amekuwa akiifanya kwa miaka 23 na anajisikia kama mtu mwenye bahati kwa kutumikia timu hiyo kwa miaka yote.
Alisema kwamba ni miaka ambayo hataisahau.
Imeelezwa kuwa Marchionne ndiye atakayechukua nafasi ya Di Montezemolo, ambaye ataondoka rasmi katika klabu hiyo oktoba 13.
Toka mwaka 2008 timu ya Ferrari haijawahi kupata ushindi ama wa udereva au wa gari lenye japokuwa wamo katika mashindano kwa miaka 20.
Jumapili iliyopita timu hiyo ilipatwa na matokeo mabaya wakati dereva wake fernando Alonzo alipolazimika kuondoka katika mashindano baada ya gari lake kupata hitilafu katika mfumo wake wa hybrid huku dreva mwingine wa timu hiyo, Kimi Raikkonen akimaliza wa tisa.
Katika miaka ya 1990 hadi 2000 timu hiyo ilitamba sana kupitia kwa dereva wake Michael Schumacher kwa kutwaa mataji mbalimbali yakiwemo ya uwezo wa gari na dereva. .